Thursday, 31 May 2012

UTU

Nina machache muhimu, ambayo ni ya thamani
Nataka kutakalamu, niyatoe hadharani
Wayafahamu kaumu, marafiki ikhuwani
Ewe kiumbe insani, kuwa mja mwenye utu

Neno ‘UTU’ tufahamu, ni funzo kwetu soteni
Nitawapa kwa nidhamu, kwa mpango wa kanuni
Na tena ni kwa nudhumu, kwa shairi kubaini
Ewe kiumbe insani, kuwa mja mwenye utu

Wema si mali ya mtu, hili tujue yakini
Wala uzuri si kitu, wa umbo lakini mwilini
Kitu aula ni utu, kitu bora duniani
Ewe kiumbe insani, kuwa mja mwenye utu

Na kivazi na kitimu, kwa utu hakilingani
Nguo si kitu adhimu, na kiatu mguuni
Kitu ni ubinadamu, kisokuwa na kifani
Ewe kiumbe insani, kuwa mja mwenye utu

Utu ni kitu adimu, kipawa chake Manani
Utu ni moyo rahimu, heshima yake insani
Na tena ni ukarimu, na roho yenye imani
Ewe kiumbe insani, kuwa mja mwenye utu

Utu sio ujabari, ushujaa wa vitani
Mtu ni utu mzuri, wa tabia na makini
Mwenye utu ni fahari, kwa wake na majirani
Ewe kiumbe insani, kuwa mja mwenye utu

Utu ni khulka njema, maumbile ya nyumbani
Ni ubinadamu mwema, ni ya Mola yake shani
Hima basi ndugu hima, utu ni wetu soteni
Ewe kiumbe insani, kuwa mja mwenye utu

Ya nane ni kaditama, kalamu naweka chini
Ikiwa niliyoyasema, nitakuwa makosani
Tafadhali kwa heshima, nawaomba msamaha
Ewe kiumbe insani, kuwa mja mwenye utu

No comments:

Post a Comment