Kwako twapomoka chini, kusudi tukuabudi
Umeijaza angani, hewa isioidadi
Mafakiri wangewaje, lau ingeuzwa hewa
Matajiri duniani, bahili
walivyozidi
Wangeitia chupani, hewa kisha wainadi
Hewa I moto thumni, na pauni ya baridi
Mafakiri wangewaje. Lau ingeuzwa hewa
Wangelia masikini, kulilia yao sudi
Hasa kwa bei sokoni, ipandishwapo zaidi
Kungezagaa huzuni, na mauko ya fuadi
Mafakiri wangewaje, lau ingeuzwa hewa
Na makwasi madukani, wangeiuza na
kodi
Uwapo huna hunani, kununua huna budi
Mana watoto nyumbani, wanakungoja urudi
Mafakiri wangewaje, lau ingeuzwa hewa
Ingetiwa na melini, iuzwe nchi
baidi
Ijengewe juu chini, mabohari ya hadidi
Bora yao ni mapeni, iende yao miradi
Mafakiri wangewaje, lau ingeuzwa hewa
Masikini uwanjani, wangepigishwa
paredi
Wapige magoti chini, kusujudia malodi
Ndipo itiwe chupani, warushiwe ja samadi
Mafakiri wangewaje, lau ingeuzwa hewa
Elakini Rahamani, achukiaye husudi
Pembe zote duniani, hewa amejaza hadi
Bure waja pumueni, bila malipo kufidi
Mafakiri wangewaje, lau ingeuzwa hewa
No comments:
Post a Comment