Nataka
kutakalamu, niyatoe hadharani
Wayafahamu
kaumu, marafiki ikhuwani
Ewe kiumbe
insani, kuwa mja mwenye utu
Neno ‘UTU’
tufahamu, ni funzo kwetu soteni
Nitawapa kwa
nidhamu, kwa mpango wa kanuni
Na tena ni kwa
nudhumu, kwa shairi kubaini
Ewe kiumbe
insani, kuwa mja mwenye utu
Wema si mali ya
mtu, hili tujue yakini
Wala uzuri si
kitu, wa umbo lakini mwilini
Kitu aula ni
utu, kitu bora duniani
Ewe kiumbe
insani, kuwa mja mwenye utu
Na kivazi na
kitimu, kwa utu hakilingani
Nguo si kitu
adhimu, na kiatu mguuni
Kitu ni
ubinadamu, kisokuwa na kifani
Ewe kiumbe
insani, kuwa mja mwenye utu
Utu ni kitu
adimu, kipawa chake Manani
Utu ni moyo
rahimu, heshima yake insani
Na tena ni
ukarimu, na roho yenye imani
Ewe kiumbe
insani, kuwa mja mwenye utu
Utu sio ujabari,
ushujaa wa vitani
Mtu ni utu mzuri, wa tabia na makini
Mwenye utu ni
fahari, kwa wake na majirani
Ewe kiumbe
insani, kuwa mja mwenye utu
Utu ni khulka
njema, maumbile ya nyumbani
Ni ubinadamu
mwema, ni ya Mola yake shani
Hima basi ndugu
hima, utu ni wetu soteni
Ewe kiumbe
insani, kuwa mja mwenye utu
Ya nane ni
kaditama, kalamu naweka chini
Ikiwa
niliyoyasema, nitakuwa makosani
Tafadhali kwa
heshima, nawaomba msamaha
Ewe kiumbe
insani, kuwa mja mwenye utu